Nafasi na Kazi ya Conductor by Richard Mloka [Sehemu ya Nne]

Inaendelea... Kama haujasoma sehemu ya kwanza, tafadhali bofya hapa > http://www.swahilimusicnotes.com/page/nafasi-na-kazi-ya-conductor-by-richard-mloka

Kama haujasoma sehemu ya pili, tafadhali bofya hapa > http://www.swahilimusicnotes.com/page/nafasi-na-kazi-ya-conductor-sehemu-ya-pili-by-richard-mloka

Kama haujasoma sehemu ya tatu, tafadhali bofya hapa > http://www.swahilimusicnotes.com/page/nafasi-na-kazi-ya-conductor-sehemu-ya-tatu-by-richard-mloka

 

SIFA ZA CONDUCTOR:
 

1. Elimu ya muziki:
Nimeweka elimu ya muziki kama sifa ya kwanza kwa sababu kwa mtazamo wangu, bila elimu kuna mambo yatavurugika. Elimu ya muziki nadharia, vitendo na utunzi ni silaha nzuri kwake. Nyimbo zinaandikwa, kwahiyo zinahitaji elimu fulani kuzisoma na kuzielewa kilichomaanishwa. Maelekezo mengi anayotoa conductor kama vile Alama ya Wakati (Time Signature) , maelekezo ya upigaji (performance expressions) ni mambo yanayohitaji elimu ya muziki. Nimeona baadhi ya conductors hawatofautishi kati ya 2 4 na 4 4, au kati ya 3 8 na 6 8. Elimu ya muziki kwa kiwango cha wastani huku kwetu itamfanya conductor awajibike vizuri. Katika nchi zilizoendelea, conductor wa orchestra anakuwa na degree ya muziki, kwao hiyo nafasi ina heshima sana.
 

2. Ufahamu wa ala mojawapo ya muziki:
Conductor anayefahamu kupiga walau ala mojawapo ya muziki anakuwa na faida ya ziada. Ala itamsaidia kuwa na ‘sikio la muziki’ na vile vile aweze kumwelekeza mpigaji wa ala hiyo nini cha kufanya katika wimbo. Akijua ala moja itasaidia kumpa picha ya mpigaji kihisia na mtazamo kuhusu wimbo.


3. Msomaji mzuri wa muziki papo kwa hapo(sight-reader):
Usomaji wa namna hii kwanza hutokana na elimu na pili, uzoefu. Akishapata elimu conductor ajizoeze kusoma nyimbo nyingi mara kwa mara ili akumbane na changamoto mbali mbali za nyimbo na vionjo tofauti kutoka kwa watunzi tofauti. Mazoezi ni jambo la msingi. Huwa nawaambia wanafunzi wangu kuwa hakuna miujiza ya mtu kuweza kusoma muziki haraka, vizuri na kwa usahihi au kupiga kinanda vizuri isipokuwa kwa mazoezi tu – practice maketh perfect!
 

4. Mdadisi na mtafiti:
Udadisi humfanya mtu ajielimishe zaidi. Udadisi ni kiu ya kutaka kujua jambo fulanikwa undani zaidi. Mtu ambae si mdadisi anaweza kubaki hapo alipo kwa miaka nenda rudi, huyu hatufai katika kuinua kikundi kimuziki kutoka ngazi moja kwenda nyingine. Conductor awe mdadisi wa kuuliza wengine wanaojua, kuhudhuria matamasha, kusikiliza nyimbo za wengine waliomzidi kiwango , kusoma vitabu na siku hizi mtandao una kila kitu, ajielimishe zaidi, asibweteke hata akisifiwa namna gani. Tena aangalie anasifiwa na nani. Mtu wa kawaida ana vigezo vya kukusifu na mtaalamu wa muziki atakusifu pia kwa vigezo, sasa inategemea unabeba zaidi sifa zipi. Ningeshauri ubebe sifa za mtaalamu wa muziki, ziwe mbaya au nzuri. Mfano. Mtu akipiga kinda kwa ‘single touch’ kutoka mwanzo wa kinanda mpaka mwisho mara moja prrrrrrrrrrrrrrrr(nadhani naeleweka, inasikika sana hii kwenye sebene zetu siku hizi) watu wa kawaida watashangilia na kusema kuwa jamaa anajua sana kupiga kinanda, lakini mtaalamu wa muziki hataona ufundi wowote hapo kwani hata panya akidondokea hizo keyboard buttons akakimbia juu yake mara moja bila shaka kinanda kitatoa mlio huo huo prrrrrrrrrrrrrrrrrr, sasa hapo tutasema kuwa panya anajua kupiga kinanda? Mtaalamu ataangalia ule uchambuzi wa noti na noti ili kuleta muziki mzuri unaowiana. Sifa zisikufanye ukose udadisi. 


5. Anayeweza kutawala hisia zake:
Kutawala hisia zote nzuri na mbaya. Hisia mbaya ni kama vile hasira, huzuni, kukata tama. Hizi hazifai hasa siku ya onesho (performance). Wanamuziki wanamsoma conductor usoni wanamwelewa hata akikasirika lakini hisia hizi (mbaya)zinapokuwa wazi mno mpaka hadhira (audience) yote ikafahamu inakuwa haipendezi. Conductors wengine hutoa maneno makali na shutuma wanapofanya onesho iwapo kuna kitu hakiendi sawa kwa wanamuziki wake. Hisia nzuri ni kama vile furaha. Conductor asifurahi kupita kiwango, akatekwa na midundo au mashangilio ya watu na kusahau kufanya baadhi ya mambo ambayo waliyafanyia kazi katika mazoezi, mfano kupunguza sauti (piano, pianissimo) yeye akapita tu sehemu hiyo kwa kujawa na furaha na shangwe ya siku hiyo.
 

6. Mtu wa watu:
Ninaposema mtu wa watu nina maana kuwa ni mtu mwenye mahusiano mazuri na wengine, mtu rahisi kushaurika, kusikiliza wengine na kujenga nidhamu ya kikundi. Kitabia awe mtu mwenye utaratibu katika mambo yake. Kuna mwingine leo anaanza wimbo huu, kesho anakuja na mwingine wakati ule wa mwanzo hajaumaliza, hafai. Awe mtu wa kuwajenga kisaikolojia wanamuziki wake. Kwenye kukata tama awape moyo, kwenye makosa asahihishe kwa upendo na uvumilivu. Asilewe sifa na asiwape sifa isiyostahili watu wake. Ajiweke katika namna ambayo watu wake wanamwelewa.

.....itaendelea