Ingia / Jisajili

Nafasi na Kazi ya Conductor by Richard Mloka [Sehemu ya Pili]

Inaendelea... Kama haujasoma sehemu ya kwanza, tafadhali bofya hapa > http://www.swahilimusicnotes.com/page/nafasi-na-kazi-ya-conductor-by-richard-mloka

Katika Sehemu ya Kwanza, nimejaribu kutaja wajibu wa conductor, ni vizuri hapa sasa niingie ndani kidogo kuangalia namna atakavyoweza kutimiza wajibu wake.


1. Kuwaunganisha wanamuziki:

Conductor anapaswa kujua aina ya muziki wanaopiga au kuimba. Anapaswa ajue pia aina ya ala za muziki zinazotumika. Nimetumia neno ala na sio vyombo vya muziki. Vyombo vya muziki (equipment) ni kama vile speaker, mixer.n.k. naongelea ala za muziki (musical instruments) kama vile ngoma, kinanda, n.k. Kwahiyo conductor anapaswa ajue jinsi atakavyowaunganisha wanamuziki (waimbaji na wapiga ala). Yeye ni kiongozi anayemtawala kila mmoja. Rafiki yangu Hekima Raymond anasisitiza kuwa ni lazima wanamuziki wamwangalie usoni hasa ishara atakazotoa kwa hisia za uzoni (facial expressions). Naam, conductor anaonyesha ishara kwa kutumia mwili wake hivyo wanamuziki ni budi wamwelewe kiongozi wao. Mfano, mpiga kinanda asianze wimbo kabla hajaruhusiwa na conductor. Conductor anaruhusu kuanza wimbo pale tu anapoona watu wake wako tayari (attentive) na sio huku mwingine anatafuta daftari, huyu mwingine anauma kucha z a vidole na mwingine ananong’ona na mwenzake. Wote wawe katika u tayari (attention).

Kazi kubwa ya conductor hufanyika wakati wa mazoezi. Kwenye mazoezi ndipo anapowazoeza kuhusu ufundi wa wimbo ( technical aspect) na hisia zinazoonekana katika wimbo. Yeye ndiye anapaswa kufanya kikundi kipige/kuimba vile anavyotaka. Anabuni (imagine) jinsi wimbo unavyotakiwa kusikika na hivyo kutumia muda wa mazoezi kufika anakotarajia, yaani jinsi alivyobuni kichwani kwake ndivyo iwe. Hapa nizungumzie mtazamo wa sanaa. Katika sanaa huwa tunaanza mwisho na kuja mwanzo. Mfano msanii mchoraji, kabla hajaanza kuchora ni lazima kwanza awe na picha anayotaka kuchora katika mawazo yake. Akishakuwa na hiyo picha kichwani ndipo anapoweza kuchora kuelekea au kufuatana na picha iliyo kichwani kwake. Kwahiyo tunaweza kusema kuwa picha ilishakuwepo kichwani kwake kabla haichora tukaiona. Karibu na nyumbani kwangu kuna kijana alifungua kiosk akamwita mchoraji achore picha ya Bob Marley. Mchoraji akafanya kazi yake, alipomaliza tukaona sio sura ya Bob Marley ila ya mwanamuziki wa Marekani Buster Rhyme! Inaonesha kuwa mchoraji hakuwa nafahamu vizuri kichwani kwake sura ya Bob Marley na kosa dogo likapelekea picha kuhamia kwa Buster Rhyme. Na conductor pia ni vizuri awe na picha ya muziki unavyopaswa usikike, wakati anausoma iwe ausikie kichwani kwake na afanyie kazi kuelekea huko, hapo anaweza kufanya mabadiliko katika wimbo hasa mwendo na hisia (tempo & dynamics)iwapo mtunzi hakuziandika au hazitoshelezi picha aliyonayo conductor wetu. Conductor asitegemee kufanya maajabu siku ya kuimba (performance) ikiwa hakuwazoeza kabla, kumbuka – ng’ombe hanenepi siku ya mnada! Tukiosikia na kuona jinsi walivyoimba na kupiga wimbo ndipo tunajua mazoezi yao yalivyokuwa, hii ni kanuni ya garbage in-garbage out!

 

2. Kuweka mwendo sawa:

Nimeelezea hapo juu kuwa conductor anaweza kufanya mabadiliko katika wimbo kuhusu mwendo. Ila ni vizuri kwanza ausome wimbo na kuelewa hisia za mtunzi kabla hajaweka za kwake. Hisia atakazoongeza zisiharibu wimbo.


3. Kuongoza maandalizi:

Conductor anasimamia vilivyo mazoezi ili, kama nilivyosema awali, siku ya tukio kitoke kile alichotarajia na si vinginevyo.
 

4. Kusikiliza kwa umakini:

Conductor mzuri ni Yule mwenye ‘sikio la muziki’. Katika mazoezi atahakikisha waimbaji na wapiga ala wote wanaimba na kupiga noti katika kiwango (pitch) na mwendo sahihi. Wakiwa jukwaani anaendelea na kazi yake ya kusikiliza na pale penye tofauti ni kazi yake kumjulisha mhusika., iwapo ni alto wanakwenda off-pitch awape ishara ili warekebishe. Sio vizuri aendelee kufurahia midundo wakati pitch inaharibika!


5. Kutengeneza sauti:

Hii ni ni kazi yake kuleta uwiano kati ya ala na sauti za waimbaji. Kama si mtaalamu wa kunoa sauti (vocal trainer) apawepo na mtaalam huyo halafu conductor atashughulikia hisia za wimbo.

 

Tutaendelea na kuona vigezo vya kuwa conductor.

Itaendelea…………